Wednesday 27 April 2011

VIPI KISUKARI KINAWAUA WATANZANIA MAARUFU?

Habari kuhusu tiba ya Loliondo zimezigusa hisia za Watanzania wengi. Huku nje suala la mzee Mchungaji Ambilikile Mwasapile; halijafahamika vizuri. Wanahabari wachache tumefuatilia mambo ya “mti wa Loliondo” mitandaoni lakini si jambo la jazba kama nyumbani.  Suala lolote linalowasaidia wanadamu kuondokana na matatizo yao ya kimaisha huwa na umuhimu katika jamii. Loliondo imewika kutokana na afya zetu kuzidi kuwa mbaya. 
Waafrika tunatafuta majibu ya haraka.

Waingereza hutumia neno “Quick Fix” kuelezea ufafanuzi wa kupinda kona. Wabrazili husema “um jeitinho” (tamka, jeichinyo) kufumbua matatizo upesi upesi. Ni kama mtu huna hela ya chai ukala kiporo. Wachagga tuna chakula kinaitwa “Ikato”  (mseto wa maharage na ndizi);  badala ya mkate au maandazi.
<--more!-->
 Ukiacha Loliondo suala la waganga wa kienyeji au uchawi ni mfano mwingine. Miaka michache iliyopita niliwahi kuandika namna jamaa wa Kiganda hapa London walivyonieleza wanavyohofia Wabongo na Juju. Kuna mmoja  akatukatia jina la Chigoma. Akasema wanaamini mkoa wa “Chigoma”  una wachawi bab kubwa. Mwingine akasema kawahi kusafiri hadi Sumbawanga na Tanga. Nikaulizwa je  mimi mzawa wa Chigoma? Nikasema natoka “Chilimanjaro.” Waganda hawasemi Kigoma wala Kilimanjaro. Juju (neno lililobuniwa  Nigeria) ni kati ya mambo yanayoheshimiwa sana Afrika.  Ikiwa uganga wa kiasili una nguvu kiasi kile mbona uhai wetu wazidi kuwa mfupi?
Takwimu za maisha ya Wana Afrika Mashariki zimelalia wastani wa miaka 40 hadi 55. Je, habari za tiba za haraka, Loliondo na Juju zinatueleza nini kuhusu jamii zetu? Je, tunafanya jambo gani la makosa tuwe tunaishi maisha mafupi vile?
Kila ukizungumza na wageni wanaokuja Tanzania watakueleza namna nchi hii ilivyo na mali asili nzuri,  udongo wa rutuba; hali ya hewa ya kuvutia bila majangwa wala barafu.  Ikiwa mazingira yetu ni tajiri vipi tunaishi maisha magumu?
Juzi nilikuwa naongea na kijana wa Kizungu aliyesafiri Afrika Mashariki kuboresha Kiswahili chake. Ingawa aliipenda Bongo (kuliko Kenya au Uganda), hata alipoibiwa Dar es Salaam (shilingi milioni saba) na majambazi pale Namanga, hakuwachukia Wabongo.
“Watanzania mna vyakula vitamu. Nakumbuka mapapai, maembe na nyama choma. Sijui kwanini mnapenda Chips na wengi hawanywi maji au kula matunda na mboga za majani.”
Kijana huyo mwenye miaka 23 bado anasoma lakini tazama alivyokuwa na mwamko kuhusu ulaji. Kwa wenzetu suala la mboga mbichi, matunda au kunywa maji limepikwa hadi likaivika katika utamaduni wao.
Ulaji sahihi ni msingi wa maisha marefu...
Maduka jamii zilizoendelea yamejaa mazao toka nchi maskini. Bidhaa hizi zisizopatikana kirahisi (maembe, mapapai, mananasi, matango, nk) ni aghali sana Majuu. Ulaji wa chakula na Salad ambao ni msingi wa milo ya Wazungu ni moja ya mambo ambayo hayazingatiwi Afrika iliyojazana mimea hiyo vichakani na mashambani. Kinachotusumbua ni kutoelewa umuhimu wa mimea hiyo na kung’ang’ania vinywaji na “vyakula vya kisasa.”
Zingatia unywaji wa Soda unavyothaminika Bongo kuliko juisi za matunda; ama ulaji wa viazi vya kukaanga (chips) zaidi ya mboga za majani. Hatuimanishi kuacha Chips au Soda, ila iko haja ya kujua namna ya kuvipanga vyakula hivi kusudi tumbo ivipokee sawasawa.
Utafiti wa miaka kumi uliofanywa na wataalamu chuo kikuu cha Wageningen, Uholanzi  baada ya kuchungua maisha ya watu 20,000 ulifikia hatima kuwa vyakula visivyopikwa (mboga  na matunda) husaidia kuzuia maradhi ya moyo na unene kuliko vile vilivyopikwa sana. Funzo hapa ni kula kila mlo na mboga  kama matango na nyanya, mathalan.
Au chumvi. Utafiti uliofanywa na maabara kadhaa Majuu karibuni umeng’amua kwamba ukipunguza chumvi katika chakula chako kwa asilia mia 25 unaongeza miaka kumi zaidi  ya maisha yako. Ina maana badala ya Mbongo kufariki akiwa na miaka 55 atabarikiwa 65 (angalau awaone wajukuu wakifunga ndoa). Zamani mababu zetu hawakutumia chumvi katika vyakula hivyo waliishi maisha marefu zaidi.
 Siku hizi ukiagiza chakula hoteli Majuu hakiji na chumvi. Inabidi ujiwekee mwenyewe mezani; hali kadhalika ukiwaalika wageni kwako kula  hukiwekei chumvi. Wenzetu wameshagundua kwamba chumvi nyingi huchangia kuziba mishipa ya damu na maradhi ya moyo. Unapopunguza chumvi unasaidia mzunguko wa damu mwilini. Chumvi  kupindukia ni ladha kuliko afya.
Ikumbukwe iwapo unatokwa sana jasho (kutokana na joto au mazoezi) ni muhimu ule chumvi. Hivyo ukila sana chumvi usisahau kunywa maji mengi ; kabla ya chakula (kama robo saa) na nusu saa kuendelea baadaye; lakini si kunywa maji mengi pamoja chakula. Hilo linaghafilisha umeng’enyaji, tumboni.
Suala jingine ni unene na mafuta. Nikiwa mdogo zamani, tulipigania sana minofu na nyama za mafuta. Ulaji wa mafuta (hususan katika nyama) na vyakula vilivyokaangwa kwa mafuta mengi, huchangia sana kunona.  Kunenepa huku  huvimbisha tumbo na kwa mtu wa makamo huning’inia  chini ya mbavu, pembe ya tumbo, nyongani unapovua nguo. Wanamichezo tumeukatia jina la “gurudumu la baiskeli.”
 Unapoanza kuona  “gurudumu la baiskeli” limekuzingira na kuwa kubwa chini ya mbavu, juu ya nyonga  jua unakaribisha maradhi kama ugonjwa wa moyo (presha), saratani ya tumbo kubwa (colon cancer) kisukari na jongo. Upo unene usioepukika unaotokana ama na kuzaliwa, uzazi (wanawake waliojifungua) au baada ya kutumia dawa fulani zinazosababisha athari hiyo. Unene tunauongelea ni ule wa kutojiangalia. Mathalan kula sana vyakula vya mafuta, tumbo likavimba na hufanyi mazoezi yeyote mfano mbio fupi, kuogelea,  mpira, mpira wa nyavu, kikapu, nk.
 Kisukari kimeshika moto Tanzania na karibuni kimeua wataalamu mashuhuri watatu: mwanamuziki Remmy Ongala (2011) wanahabari Mike Sikawa (2008) na Adam Lusekelo (2011). Zipo aina mbili za kisukari ila kinachosumbua wengi ni  “Type 2 Diabetes” inayosababishwa na ulaji mbaya, pombe na kutofanya mazoezi.   Tatizo hili limeenea duniani hasa nchi tajiri kama Dubai.
Miaka minne iliyopita mganga mkuu wa Dubai, Dk. Abdul razzak Ali Madani alitangaza serikali yake hutumia asilimia 40 ya kipato kutibu wagonjwa wa kisukari. Jamii hiyo ina maisha mazuri kiasi ambacho wanananchi wamejiachia, hawafanyi mazoezi, wanatembea kila mahali na magari.  Kutokana na tatizo tarehe 4 hadi 8 Desemba mwaka huu mkutano wa kimataifa wa maradhi ya Kisukari utafanyika Dubai. Sina hakika kama Watanzania tutawakilishwa au la.
  
-London, Jumanne, 12 Aprili, 2011.


Ilitoka  gazeti la Mwananchi 17 Aprili, 2012. Sidhani ilinukuliwa katika mtandao wao baadaye ndiyo maana imeuliziwa sana humu...





1 comment: